Saturday, September 1, 2012

WATU WENGI HAWAJAFIKIWA NA MAKARANI WA SENSA MKOANI MBEYA


Kamishna wa Sensa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)  Hajjat Amina Mrisho Said akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu zoezi la Sensa ya watu na makazi 2012  linaloendelea nchi nzima na kutoa wito kwa wananchi ambao bado hawajahesabiwa kutoa taarifa kwa viongozi wa serikali za mitaa.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Kamishna wa Sensa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Hajjat Amina Mrisho Said (hayupo pichani) leo jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya kuongezwa kwa muda wa zoezi la Sensa ya watu na makazi litakalomalizika tarehe 8 Septemba 2012.


Na, Gordon Kalulunga.

WAKATI Kamishna wa Sensa wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS)  Hajjat Amina Mrisho Said akitangaza kuongeza siku za sensa kuwa ni mpaka Septemba 8 mwaka huu, wananchi wengi mkoani Mbeya hawajafikiwa na makarani wa Sensa.

Uchunguzi uliofanywa na mtandao wa www.jamiiyetu2012.blogspot.com umebaini kuwa baadhi ya makalani hata hawashirikiani na Wenyeviti wa Mitaa/Vitongoji huku wengine wakiwa wameishiwa vifaa vya kuhesabia.

Wananchi wengi wamelalamikia zoezi la Sensa linaloendelea ambapo wananchi wa Kijiji cha Ndola kata ya Nsalala Wilaya ya Mbeya Vijijini Mkoani Mbeya wamesema kuwa ni asilimia 20 tu ya wakazi wa Kijiji hicho ndiyo waliohesabiwa.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mzalendo katika Kijiji hicho Jackson Mwasenga (Chadema) amesema kuwa katika Kitongoji chake ni wananchi wachache waliohesabiwa huku makarani wa Sensa wakiwa wameishiwa vifaa.

Alisema imefika mahala wananchi wanawaendea viongozi wakitaka kuhesabiwa ili hali viongozi hao hawana hata mafunzo ya zoezi lenyewe jambo ambalo amelitafsiri kuwa Serikali inawachonganisha viongozi hao na wananchi. 

Mbali na Kijijiji hicho, pia katika Kijiji cha Mbalizi wilayani humo na maeneo kadha ya Jiji la Mbeya wananchi wamelalamikia kutofikiwa na makarani hao wa Sensa.

Wananchi hao wameiomba Serikali kupeleka vifaa hivyo vya sensa kwa Mabalozi na wenyeviti wa Mitaa/Vitongoji maana wao ndiyo wanawajua wakazi wa maeneo husika kuliko hivi sasa zoezi hilo limeendelea kufanywa kwa hali inayotafsiliwa kuwa ni kama kuna kificho.

No comments:

Post a Comment