WAKATI Serikali ikitafakari jinsi ya kurudisha nyumba zake zilizouzwa kwa watu binafsi kote nchini, nyumba nyingine ya Serikali imeuzwa Jijini Mbeya kwa mfanyabiashara maarufu hapa nchini, imebainika.
Nyumba hiyo iliyopo eneo la Mafiati yenye namba 162 block S, licha ya Wakala wa majengo mkoa wa Mbeya kuzuia kuuzwa, kampuni ya udalali ya J.A. Kandonga Court Broker $ Publicationerer ilikaidi na kuiuza.
Nakala ya Barua ya wakala wa majengo mkoa wa Mbeya ya Julai 4, mwaka huu iliyopelekwa kwa dalali huyo, imesema kuwa inasikitika na tangazo la dalali huyo kuhusu kukusudia kuiuza nyumba hiyo kutokana na amri ya Mahakama.
Barua hiyo ambayo imesainiwa na kaimu wa wakala huyo mkoa wa Mbeya Mhandisi Jafari Kiyoga, imesema kuwa kwa taratibu za kiserikali nyumba hiyo isingepaswa kuuzwa kutokana na mikataba ya kisheria ya ununuzi wa nyumba za Serikali ambapo sheria inaruhusu nyumba hizo za Serikali kuuzwa baada ya miaka 25 tangu kutolewa kwa hati miliki.
Barua hiyo imenukuliwa ikisema kuwa Ofisi ya wakala wa majengo ilisikitika kumtaarifu dalali huyo kuwa tangazo lake ni kinyume na mkataba wa mauziano ya nyumba kati ya Serikali na mtumishi husika.
''Kwa mujibu wa mkataba wa mauziano kifungu Na, 9 na 10, mtumishi aliyeuziwa nyumba au mrithi wake haruhusiwi kuiuza nyumba hiyo mpaka hapo itakapotimia miaka ishirini na tano (25) kuanzia tarehe ya hati miliki'' imesemam barua hiyo yenye kumbu kumbu namba MID/TBA/MBY/GH 162 'B'/8
Vyanzo vyetu vya habari kutoka kwenye mamlaka mbalimbali vilisema kuwa nyumba hiyo imeuzwa kwa Sh. Milioni 250 kwa mfanyabishara maarufu nchini mkazi wa Jijini Dar es Salaam ambaye ni mzaliwa wa mkoa wa Mbeya.
Mtumishi aliyekuwa ameuziwa nyumba hiyo awali na Serikali Simboleo Gibson Kileo alipotafutwa kuthibitisha kuwa nyumba hiyo imeuzwa alikiri kuuzwa kwa nyumba hiyo kinyume cha sheria.
Alisema nyumba hiyo aliinunua mwaka 2002 na kumalizia fedha za nyumba hiyo mwaka 2005 na kasha kupatiwa hati miliki mwaka 2007 na kwamba alishangazwa na dalali huyo kufika eneo la nyumba na kuwakwepa watu waliokuwepo kwa ajili ya kuinunua nyumba hiyo lakini dalali aliondoka na kurejea baadae na kuwatangazia watu kuwa nyumba hiyo tayari ilikuwa imenunuliwa kwa Sh.Milioni 250 huku wengine walikuwa tayari kuinunua kwa Milioni 400.
Kwa upande wa viongozi wa kampuni ya udalali ya Kandonga walipopigiwa simu hawakuweza kupatikana.
No comments:
Post a Comment