NAIBU Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema wabunge wengi ni waongo na wamekuwa wakitumia upenyo wa Bunge kutamka maneno yasiyo na ukweli kwa uwazi kabisa.
Aliyasema hayo juzi usiku wakati akizungumza katika kipindi cha ‘Dakika 45’ kinachorushwa na televisheni ya ITV.
Ndugai ambaye alikuwa akizungumzia juu ya malumbano na misuguano ambayo imekuwa ikiibuka bungeni, alisema mengi yamekuwa yakianzia kwenye majukwaa ya kisiasa, na kwamba wakitoka huko wanayahamishia bungeni.
Katika hilo alisema imesababisha wabunge wengi kusema uongo kwa uwazi, huku wakiwataja watu wengine ndani ya Bunge hali ambayo imeliletea usumbufu Bunge lenyewe na watu katika familia zao.
“Wabunge wanawataja watu wengine kwa majina na kuwasingizia uongo…wananchi wamekuwa wakitupigia simu. Sasa hili si zuri, kwa kweli linatusumbua,” alisema Ndugai.
Mbali na hilo, Ndugai ambaye ni mbunge wa Kongwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alizungumzia pia kuhusu lugha za matusi na vijembe, ambazo zimekuwa zikitumiwa na baadhi ya wabunge kwa sababu tu ya chuki binafsi na za kisiasa.
Aliwakumbusha wabunge akisema wanapaswa kuisimamia serikali kwa lugha ya staha na si ya matusi, huku akiwataka kurudi katika misingi ya lugha ya kistaarabu.
Kuhusu matumizi ya kanuni ya kutaka muongozo au utaratibu, ambazo zimekuwa zikisababisha malumbano makubwa baina ya wabunge wa chama tawala na wale wa upinzani, Ndugai alisema kanuni hizo ziliwekwa kwa nia njema.
Alisema mbunge anatakiwa kuomba mwongozo endapo kuna jambo limetokea ambalo si la kawaida.
Aidha, kuhusu kanuni ya kuomba taarifa, alisema mbunge anaweza kuomba taarifa endapo mbunge anayeongea anapotosha na kuongeza kuwa, kanuni hizo na nyingine zimewekwa ili Bunge liendeshwe kwa usahihi, lakini badala yake zimekuwa zikitumiwa vibaya kwa nia ya kukomeshana, kurushiana vijembe, kudhoofisha hoja ya mbunge mwingine au kuipoteza kabisa.
“Hili jambo lina changamoto kubwa, wananchi wanatupigia simu wanatuuliza mbona yule ulimnyima mwogozo…kuna watu wana nia ya kukashifu wanakuwa wamepanga kabisa tangu huko nje, sasa mtu huyu akivunja kanuni ukimtoa nje anaonekana shujaa na magazeti yote yanaandika… mimi nafikiri kanuni hizi huku mbele zitazamwe upya… ikiwezakana adhabu ziongezwe ili kuleta heshima ya Bunge,” alisema Ndugai ambaye hata hivyo alisisitiza kuwa bado Bunge lina rekodi safi.
Ndugai ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti katika Bunge la tisa wakati Samuel Sitta akiwa spika wake, alisema wakati akishikilia nafasi hiyo hakuwahi kumtoa mbunge hata mmoja nje, lakini tangu awe naibu spika amewatoa wabunge wengi.
Kuhusu eneo ambalo Bunge lilipata wakati mgumu katika mkutano wa bajeti uliomalizika mwezi uliopita, Ndugai alisema ni wakati wakipitisha bajeti za wizara takribani nne ambazo ni za Nishati na Madini, Wizara ya Maji, Elimu na Uchukuzi.
Kwa mujibu wa Ndugai, wizara hizo ziliwapa tabu kwa sababu zinagusa matatizo waliyonayo wananchi kwa mfano, umeme, maji, usafiri wa reli na majini, pamoja elimu ambayo wananchi wanalalamikia ubora wake.
Hata hivyo alisema kati ya wizara hizo zote, waliyopata nayo tabu zaidi ni Nishati na Madini ambayo ina matatizo makubwa ya mambo ya TANESCO na madini.
“Hii wizara sio sasa tu tumepata nayo shida, ni miaka yote, kila mwaka bado ni matatizo, sasa linakuja suala la gesi ambalo nalo linaigusa wizara hii hii… ni eneo ambalo wabunge wamekuwa wakipendekeza mara zote kwamba igawanywe,” alisisitiza Ndugai.
Kuhusu Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa na Spika Anne Makinda hivi karibuni kwa tuhuma za rushwa, Ndugai alisema kulikuwa na mvumo wa madai yasiyothibitika kwamba wajumbe wake walikuwa hawaaminiani na walikuwa na mahusiano yasiyo ya kiafya na Wizara ya Nishati na Madini, kadhalika TANESCO.
Alisema kwa sasa bado Kamati ya Maadili ya Bunge inapitia madai ya rushwa pamoja na kuchunguza, na kwamba ikithibitika mbunge anaweza kupoteza ubunge wake na hata kujikuta katika vyombo vya sheria.
Ndugai alisema kamati haitamfumbia macho yeyote na kuvitaka vyama vya siasa kuwapa ushirikiano katika suala hilo ili hata pale wabunge wao watakapothibitika waweze kuchukuliwa hatua zinazostahili.
Kuhusu sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii ambayo nayo iliibua mjadala mkali katika Bunge la Bajeti, Ndugai alielekeza lawama moja kwa moja kwenye Kamati ya Jamii Jinsia na Watoto, akisema ndiyo iliyopaswa kuliangalia suala hili kwa mapana kabla ya kulifikisha katika vikao vya Bunge ambako linapata muda mdogo sana kutizamwa.
“Mabadiliko haya pia katika Bunge yanakuja siku za mwisho na wabunge wanakuwa na haraka… tunahitaji wadau nao washirikiane na sisi pale tunapowaita kwenye kamati waje washauri ili kuboresha mambo kama haya… kamati ina nafasi kubwa ya kusaidia kwa sababu inapata muda mrefu wa kutazama tofauti na muda wa Bunge…labda tu niwahakikishie wananchi kwamba Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo (CCM) ameleta hoja tuiangalie, tutaiangalia,” alisema.
Alisema kadhia nyingine ambayo inasababisha mambo kama hayo yafike hapo ni ule utaratibu wa kufanya mabadiliko madogo katika sheria ambako wakati mwingine huleta shida.
|
No comments:
Post a Comment