Wednesday, September 5, 2012

Wanafunzi darasa la tano wajiunga na Sekondari

* REO, Walimu wakiri, Waziri hajui lolote
 
 
Na, Gordom Kalulunga, Mbeya
 
WANAFUNZI wengi wanaosoma katika shule za michepuo ya Kiingereza ( English Medium School ) wanajiunga na Sekondari wanapomaliza kufanya mitihani ya darasa la tano na sita, imethibitika.
 
 
Uchunguzi uliofanywa kwa muda wa miaka miwili sasa, umebaini kuwa wazazi wengi kwa kushirikiana na walimu wa shule hizo, wamekuwa wakiwatoa wanafunzi wale ambao wanaonekana kuwa na uwezo kimasomo na kuwapeleka kwenye usaili wa kujiunga na shule za Sekondari za binafsi zikiwemo za Wazazi wakifaulu wanaendelea kusoma masomo ya Sekondari.
 
 
 
Hali hiyo kwa mkoa wa Mbeya na nchi nzima kwa ujumla, imeendelea kuota mizizi kwa miaka zaidi ya mitatu sasa, ambapo shule nyingi za Sekondari hasa zile zinazofaulisha vema zimekuwa zikipokea wanafunzi hao bila kujua.
 
 
 
Baadhi ya wakuu wa shule za michepuo ya kiingereza walioomba hifadhi ya majina yao na majina ya shule wanazofundisha waliohojiwa walikiri kuwepo kwa hali hiyo na kwamba kwa sasa hali hiyo imekuwa ni kawaida.
 
 
‘’Ni kweli hali hiyo kwa sasa imezoeleka na ndiyo maana hata wanafunzi wanaohitimu darasa la saba katika shule zetu hizi wanakuwa wachache tofauti na wanaokuwa wameanza na tunawaona watoto hao wanaendelea na masomo ya Sekondari lakini tunakuwa hatuna jinsi’’ walisema walimu hao.
 
Nao baadhi ya wakuu wa shule za Sekondari za binafasi waliohojiwa walikiri kuwepo kwa tabia hiyo na kudai kuwa wao wakati wa kusaili wanaangalia uwezo wa mwanafunzi na wala hawahoji kama mtu alimaliza lini darasa la Saba .


Baadhi ya wazazi ambao tayari watoto wao wapo katika Sekondari mbalimbali nchini wakitokea madarasa ya tano na sita katika shule za michepuo hiyo ya kiingereza walisema kuwa waliwapeleka watoto wao shule hizo kutokana na uwezekano mkubwa wa watoto wao kuhitimu masomo wakiwa wadogo kuliko wangewapeleka shule za Msingi za Serikali ambako watoto wao wasingeweza kufanikiwa katika zoezi hilo.
 
 
 
Kwa Upande wake Afisa Elimu wa mkoa wa Mbeya Juma Kaponda alipotafutwa ofisini kwake hakuweza kupatikana na alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu jambo hili alikiri kupata taarifa hizo na kwamba miaka mitatu iliyopita alilikemea jambo hilo na kumrudisha mmoja wa mwanafunzi aliyebainika katika shule ya Sekondari ya Sangu iliyopo Jijini Mbeya.
 
 
‘’Ni kweli nimewahi kupata taarifa hizo na tuliwahi kumrudisha mwanafunzi mmoja shule ya St. Marys aliyekuwa ameanza masomo ya Sekondari katika shule ya Sangu na bada ya hapo nilikaa na wakuu wa shule za Msingi na Sekondari na kukemea jambo hilo na baada ya hapo sijawahi kupata taariza zaidi.
 
 
Alisema kitendo hicho ni kosa kisera na kisheria na kwamba sera inaruhusu mwanafunzi kurushwa madarasa endapo atathibitika kuwa ana uwezo mkubwa darasani ambapo taratibu zinazotakiwa kufuatwa ni mkuu wa shule ya Msingi kumwandikia barua Afisa Elimu wa wilaya, afisa wa wilaya kumwandikia Afisa elimu wa mkoa na Mkoa humwandikiwa barua Kamishna ambaye akithibitisha ndipo hutoa ruhusa na si vinginevyo.
 
 
Aliongeza kuwa kumrusha mwanafunzi madarasa si jambo jema kwasababu humpunguzia vitu Fulani mwanafunzi husika kwasababu Darasa la Saba kuna miongozo ya kumwandaa mwanafunzi kwenda kidato cha kwanza.
 
 
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na mafunzo ya Ufundi Phillip Mullugo alipohojiwa alisema kuwa hana taarifa yeyote na hajawahi kulisikia jambo hilo ambapo alisema kuwa kama lipo na likathibitika atalishughulikia.
 
 
 
Imebainika kuwa wanafunzi hao wa darasa la tano wanaotoka shule za michepuo ya kiingereza wanakuwa na uwezo mkubwa wa kimasomo ikiwemo kusoma na kuandika tofauti na wale wanaosoma katika shule za Serikali ambao baadhi yao licha ya kufaulu na kwenda katika shule za Sekondari wanakuwa hawajui kusoma na kuandika.

No comments:

Post a Comment