CHAMA cha walimu Tanzania (CWT) kimempa siku saba Mkuu wa wilaya ya Mbeya Dr. Norman Sigalla kwa madai kuwa aliwakashifu walimu na chama hicho kwa ujumla wakati wa semina za Senza ya watu na makazi hivi karibuni.
Taarifa yenye kumbu kumbu namba CWT/MBY/MW/VOL.II/57 iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari mkoani Mbeya na katibu wa CWT mkoa wa Mbeya Mwl. Kasuku Bilago ilisema kuwa (CWT) mkoa wa Mbeya kilipokea toka kwa walimu malalamiko juu ya Mkuu huyo wa wilaya jinsi alivyowakashifu wakati wa zoezi la semina za sensa ya watu na makazi.
Ilisema kuwa kwa nyakati tofauti, Mkuu huyo wa wilaya alipita kwenye vituo vya semina hizo ambazo wengi walikuwa walimu na kutoa kashifa dhidi ya walimu na taaluma yao pamoja na CWT.
Taarifa hiyo ambayo ni barua ambayo aliandikiwa Mkuu huyo wa wilaya Agosti 21 mwaka huu imeeleza kuwa baadhi ya kashifa alizotoa zilisema walimu ni kada ya waliofeli mitihani na hivyo serikali inawashangaa kudai waongezewe mishahara.
‘’Ulieleza kuwa walimu wamejaa madudu kichwani, Ulieleza kuwa walimu ni manjuka yaani watu mbumbumbu wasiojua kitu chochote, Ulikuwa ukiwaeleza walimu kuwa Mukoba (Rais wa CWT) anamiliki pesa nyingi toka CWT hivyo hata akigoma na kufukuzwa kazi hatapata shida yoyote ya maisha, hivyo anawadanganya walimu wanaogoma’’ imeeleza taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa Mkuu huyo wa wilaya alieleza kuwa CWT kinawanufaisha makatibu na viongozi kuliko walimu maana wao wanatembelea magari kwa pesa zao na hivyo ni kwa nini walimu waigomee serikali badala ya kukigomea chama chao CWT.
Alikuwa akieleza kuwa washiriki wa semina hawatakiwi kuugua, kufa wala kufiwa kabla ya zoezi la sensa kuisha ila baada ya sensa wanaruhusiwa kuugua, kufa na kufiwa maana serikali haitakuwa na hasara yoyote.
‘’Kwa mantiki hiyo, walimu wametafakari na kuona kuwa kauli hizo ulizotoa kwao tena wakiwepo washiriki wengine wasio walimu zimewadhalilisha, kuwafadhaisha na kuwafanya wadhaulike kwenye jamii na hivyo kuathirika kisaikolojia. Aidha, CWT kimeona kuwa ulikuwa na lengo la kuvuruga zoezi zima la sensa ya watu na makazi kwani uliondoa utulivu wa washiriki wa semina na kuwafanya wajadili zaidi juu ya kauli zako zenye kila aina ya maudhi’’
Bilago alisema CWT hakiwezi kuvumilia viongozi wa serikali wa aina hii wasioheshimu na kuthamini walimu waliowafundisha na waliopewa dhamana ya kuelimisha umma wa nchi hii. Aidha, CWT kinajiuliza kama Mkuu huyo wa wilaya alipoteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Mbeya alitumwa kuwakashifu walimu? Na kwamba Je, sera anazotekeleza kweli ni za Chama tawala au ni za kwake mwenyewe?
Hivyo kutokana na hali hiyo walimu na chama chao kimemtaka ili warudishe moyo wa kuendelea kumwamini awaombe radhi walimu ndani ya siku 7 kwa kila kituo cha semina ya sensa na makazi ya watu alichopita na kutoa kauli hizo, amuombe radhi Rais wa CWT mwl. Gratian Mukoba ndani ya siku 7 na awaombe radhi makatibu na viongozi wa CWT ndani ya siku 7 aliodai wanajinufaisha na CWT kuliko kuwanufaisha walimu.
Na kwamba kama atashidwa kufanya hayo matatu, CWT kitaingia kwenye hatua nyingine zaidi kwani walimu walioathirika na kauli hizo wako tayari kwa hatua yoyote itakayochukuliwa na CWT.
Barua aliyoandikiwa Mkuu huyo wa wilaya imesambazwa nakala zake kwa Waziri Mkuu, Katibu Mkuu CWT, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkuu wa Mkoa na Makatibu CWT Mkoa wa Mbeya.
No comments:
Post a Comment