CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimekiri kufadhiliwa kutoka nje ya nchi katika shughuli zake za kujijengea uwezo.
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema hayo jana katika semina iliyoshirikisha baadhi ya viongozi wa chama hicho na wageni kutoka shirika la Chama cha Kikristo cha Ujerumani (CDU) la Konrad Adenauer Stiftung (KAS). Kwa mujibu wa Dk Slaa, Chadema na KAS, wamekuwa na ushirikiano wa karibu kwa miaka sita sasa na ushirikiano huo umelenga zaidi kukuza demokrasia nchini.
Dk Slaa alidai kuwa Chadema ni chama chenye uwazi kwa kila mtu na katika uhusiano wao na KAS, hakiletewi fedha moja kwa moja kwa ajili ya operesheni au maandamano, ila kujijenga kiuwezo.
Pamoja na kusema kuwa KAS haitoi fedha moja kwa moja kwa Chadema kwa ajili ya maandamano na kampeni, lakini Dk Slaa alidai kuwa shirika hilo huwasaidia wastani wa Sh milioni 60 kwa mwaka kwa ajili ya machapisho na kutoa elimu.
Pia amesema kipo chama cha Uholanzi ambacho hakukitaja jina, lakini akakiri kuwa huwafadhili Sh milioni 20 kulingana na idadi ya wabunge walio bungeni. Pamoja na kusema kuwa ni kawaida kwa vyama vya mrengo mmoja kusaidiana duniani, Dk Slaa alisema chama hicho cha Uholanzi kinachowasaidia, pia hufadhili CCM fedha zaidi ya zinazopelekwa Chadema kutokana na chama hicho tawala kuwa na idadi kubwa ya wabunge.
Mbali na hilo Dk Slaa amedai kwamba kwa kuanzia wameamua kumshitaki Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye. Kwa mujibu wa madai ya Dk Slaa, tayari Chadema imefungua kesi namba 186 ya mwaka 2012, katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam dhidi Nape, ambaye anadaiwa alitamka Chadema kufadhiliwa kutoka nje. Dk Slaa amedai kuwa kesi hiyo itakapokuwa ikiendelea, wataongeza watu wengine walioeneza kauli hiyo.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema ili uchumi uwe endelevu, lazima wananchi wapewe haki na kuruhusu sekta binafsi kusimamia uchumi na si rahisi kusimamia uchumi kwa sera za kijamaa.
CHANZO: HABARILEO
CHANZO: HABARILEO
No comments:
Post a Comment