Saturday, September 1, 2012

JK Wasaidie Kawambwa na Mulugo kurejesha kusoma na kuandika

RAIS WA TANZANIA JAKAYA KIKWETE

NA, GORDON KALULUNGA

NATAMBUA fika kuwa elimu nzuri inatokana na mitaala mizuri, vifaa vya kutosha vya kufundishia na ikama nzuri ya walimu katika shule hasa elimu ya Msingi na Sekondari.

Sitaki kuamini kuwa walimu wa elimu za vyuo vikuu ndiyo wenye uwezo mzuri wa kufundisha bali ninachokiamini ni kwamba mwalimu aliyesomea mbinu bora za kufundisha ndiye chachu ya kupatikana kwa elimu bora.

Nalisema jambo hili kwasababu wengi tuliosoma miaka ya nyuma tulifundishwa na walimu waliokuwa wakijulikana kama walimu wa UPE ambao binafsi nawamwagia sifa zote za heshima za kuitwa walimu kutokana na uzalendo waliokuwa nao kwa Nchi.

Hakuna ubishi kuwa matunda yao yalikuwa yakionekana wazi wazi kwa wanafunzi wao ambao walikuwa na uwezo wa kuandika hata barua za kazi walipofika darasa la Nne tofauti na hivi sasa.

Matunda ya walimu wangu hao waliokuwa wakiitwa wa UPE hayakuishia hapo bali yalioneka pia hata Bungeni kwa kutamka matamko ya kupambana na maadui ujinga, umasikini na maradhi ikiwa ni pamoja na kuandaa mitaala mizuri ya elimu kwa watanzania. Hakika tulinufaika.

Wazazi hawakuwa na haja hata ya kutupeleka katika shule za nje ya nchi maana tulichokuwa tukikipata kwa walimu wetu wenye uzalendo kilikuwa kikionekana na ndiyo maana hata wanakijiji walikuwa wakiwapelekea hata mayai na maziwa kama motisha walimu hao maana kwanza walikuwa wakijiheshimu ndiyo maana jamii nayo ilikuwa ikirudisha heshima kwao.

Katika makala hii namtwisha mzigo Rais Jakaya Kikwete kuwa kwasababu watanzania ndiye tuliyemwamini kuendesha nchi kama kiongozi mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umefika wakati kufumba macho na kuiokoa elimu hasa elimu ya Msingi ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi.

Wizara hii inaongozwa na watu wengi kiutendaji wakiwemo makatibu lakini Waziri wake ni Dr. Shukuru Kawambwa na Naibu wake ni Philip Mullugo ambao siamini kuwa wameishindwa Wizara hiyo bali ninachokiamini ni kwamba mfumo wa mapokeo walioukuta unaendelea kuwatafuna.

Mfumo huo ni pamoja na mtaala unaowaonesha kuwa watoto wadogo wanaoanza darasa la kwanza ni lazima wasome masomo Saba ambayo katika masomo hayo somo la kusoma na kuandika halipo. ‘’Inasikitisha sana’’

Hivi karibuni Naibu Waziri wa Elimu Phillip Mullugo alitamka kuwa inapaswa wanafunzi hao wapunguziwe idadi ya masomo kutoka masomo Saba mpaka matatu ambayo bado hakufafanua kuwa yawe ni masomo yepi.

Kuna mahala Tanzania imepasuka kuhusu elimu, kwa mfano Serikali imekubali mapokeo ya mfumo wa kutumia mshine kusaisha mitihani na kuachana na mfumo wa walimu kuhusika kusaisha mitihani hiyo ambapo kutokana na mashine hizo zilivyotengenezwa zinasahisha herufi na kuwalazimisha watanzania kutunga hesabu za majibu ya kuchagua!

Dosari ya kwanza ni kutokuwa na somo la kusoma na kuandika tofauti na zamani wanafunzi tulikuwa tukigawiwa na vibao vya kuandikia, lakini asa hakuna vibao wala chaki za kutosha kwa walimu huku hata fedha za Capitation zinatolewa mashuleni kama anasa! Kuna mahala Tanzania imepasuka.

Dosari ya pili na matokeo yake ni kupata kizazi cha ‘’Masharobalo’’ wasiojua kusoma na kuandika kwasababu hata kabla ya kufanya mitihani wanakuwa na uhakika wa kufaulu kwasababu hata mwanafunzi akijaza maswali yote kuwa majibu yake ni herufi ‘’A’’ lazima atapata na mashine zinazoitwa za kisasa zitampatia alama ya vema.

Kutokana na mitaala hiyo ambayo inapewa majina mengi likiwemo jina la mitaala ‘’mibovu’’ ambayo mimi bado sijaitafutia jina angalau linaloweza kufikisha hisia zangu za kutopendezwa nayo, imefikia kwa sasa wanafunzi hawajui hata kuandika Imla ambayo ni kipimo pia cha mtoto kama anajua ama kuelekea kujua kuandika.

Niseme wazi kuwa, ili kuokoa elimu yetu hapa Tanzania Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuingilia kati suala hili na haraka iwezekanavyo somo la kusoma na kuandika lirejeshwa kwa darasa la kwanza na darasa la pili ili kuweza kuweka msingi imara wa watanzania kujua kusoma na kuandika kwanza.

Wakati masomo hayo ya kusoma na kuandika yanarejeshwa, haraka iwezekanavyo ni muhimu shule hizo zikapalekewa vifaa vya kutosha vikiwemo vibao vya kuandikia wanafunzi ambavyo kila kimoja kinakatwa kwa kwa squarmeter pembe nne sawa ambavyo vinatokana na Siling boad ambavyo vimepakwa rangi.

Sambamba na vibao hivyo shule hizo za umma zipelekewe Chaki za kuandikia kwasababu Riport ya uchunguzi uliofanywa na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Tanzania Community Media Organization (TACOMO) katika mikoa ya Nyanda za juu kusini inaeleza kuwa upatikanaji wa chaki katika shule za Msingi ni kama anasa ambapo walimu wanapoenda madarasani kufundisha huesabiwa chaki na wakuu wao wa shule.

Rais wetu Jakaya Kikwete, kwa kauli yako au maelekezo yako jinsi itakavyokupendeza, ukiyafanya hayo kwa usimamizi usio na watendaji ‘’michwa’’ hatutasikia tena taarabu hizi za kuwa na wanafunzi wa kidato cha kwanza ambao hawajui kusoma na kuandika.

Ili kumuenzi kwa vitendo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni muhimu tukafuta aibu hii ya kuwa na wanafunzi wanaohitimu elimu ya Msingi ambayo ndiyo elimu Mama pasipo kujua kusoma na kuandika.

Kuna siasa za kwamba watoto hao wanajifunza kusoma  na kuandika wanapokuwa katika shule za awali ‘’Chekechea’’ jambo ambalo halina uhalisia na matunda yake ndiyo haya tunayoyaona ya watanzania waliohitimu elimu za Msingi kubainika kuwa hawajui kusoma na kuandika…inauma sana na jambo hili halina heshima hata kidogo na ndiyo maana nasema kuwa Rais Kikwete wasaidie Kawambwa na Mulugo kurejesha kusoma na kuandika.

Mwandishi wa makala anapatikana kwa simu 0754 440749

No comments:

Post a Comment