Na Venance Matinya, Mbeya.
MKUU wa Wilaya ya Mbarali Gulamu Hussen Kiffu amenusurika kuumizwa na wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha Chimala kilichopo Wilayani humo baada ya kuvamia gari lake na kuvunja vioo,kutoa upepo wa matairi kutokana na Serikali kufunga chuo hicho kwa kutokuwa na hadhi ya kudaili wanafunzi.
Kutokana na vurugu hizo zilizotokea chuoni hapo juzi jioni, Jeshi la polisi Mkoani Mbeya linawashikilia wanafunzi sita akiwemo Mkuu wa Chuo hicho Francis Mtega kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu zilizopelekea kuharibu gari la Mkuu wa Wilaya ya Mbarali.
Kamanda wa polisi Mkoani hapa Diwani Athuman alisema baada ya mkuu wa wilaya kuongozana na baadhi ya viongozi wa serikali hususani kamati ya ulinzi na usalama wilaya kwa lengo la kutaka kujua sababu za chuo hicho kuendelea kufundisha wakati serikali ilitoa agizo kifungwe ndipo hapo walipovamiwa na wanachuo hao.
Alisema tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya kuwasili Chuoni hapo kwa lengo la kuzungumza na uongozi wa chuo ndipo baadhi ya wanafunzi walivamia gari la Mkuu wa Wilaya na kuanza kuvunja vioo kwa kutumia mawena kisha kutoa upepo kwa malengo yasiyojulikana.
Kamanda Athumani alisema tukio hilo linaonesha ni mpango uliokuwa umepangwa na uongozi wa Chuo kwa muda mrefu kwani serikali ina malengo mazuri kwa watanzania na lengo kuu ilitaka chuo hicho kisajiliwe ili kitambulike na Serikali na kuweza kutoa wauguzi walio na sifa na kuwawezesha kupata ajira itakayotambulika serikalini.
Aliongeza kuwa kitu cha kushangaza ni madaraka aliyonayo mkuu wa chuo hicho ambapo yeye mwenyewe ni mwalimu na mhasibu na kwamba kulikuwa hakuna sababu ya kufanya vurugu bali kilikuwa ni kitu cha kutoa vielelezo vya udaili wa chuo.
Alisema katika uchunguzi wa awali umebaini kuwa chuo hicho kimeanza muda mrefu na tayari kimeweza kutoa wauguzi katika Nyanja mbalimbali bila ya serikali kutambua kama hakijasajiliwa na hakitambuliki.
“ Kutokana na vurugu hizo wanafunzi 32 wanashikiliwa na Jeshi la P[olisi ambapo kati ya hao watano ndio waliobainika kuhusika na vurugu hizo na wanatarajiwa kufikiswa mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zinazowakabili ili sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine” alisema Kamanda huyo.
Aliwataja wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Mkuu wa Chuo Francis Mtega, Steven Mapunda (19), Isaya Katuwa (23) , Lugano Mwalupasya (22), Emmanuel Bukuku (24) ambao wanatarajia kufanya mtihani wiki ijayo ya kuhitimu mafunzo ya uuguzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbarali Gulamu Hussen Kiffu alikiri kutokea kwa vurugu hizo zilizotokana na uamuzi wa serikali kufunga chuo hicho kutokana na kutokuwa na sifa ya kufundisha na kudaili wanafunzi wa fani ya uuguzi kwani kilikuwa hakina hati ya utambulisho wa usajiri serikalini.
Kiffu alisema kuwa baada ya serikali kutambua tatizo hilo ndipo walipo mwita Mkuu wa Chuo hicho Francis Mtega katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambapo aligoma kuhudhuria na kueleza kuwa yeye anaendelea kufundisha ndipo walipolazimika kufika chuoni hapo.
No comments:
Post a Comment