Wednesday, September 5, 2012

Utata waibuka ujenzi wa Soko la Mwanjelwa Mbeya

 
·       Mafundi waeleza ujenzi holera, Jiji wapuuza
·       Tamisemi watoa mtihani ofisi ya mkoa Mbeya
·       Polisi wafuatilia, Mbunge Sugu aguna
 
 
 
SOKO jipya la kisasa la Mwanjelwa Jijini Mbeya linalojengwa na mkandarasi Tanzania Building Works (TBW) baada ya kuteketea Desemba, 2006 limeelezwa kuwa halina ubora uliotarajiwa na kufadhiliwa na benki ya CRDB.
 
Uchunguzi uliofanywa kwa muda wa miezi sita sasa, umebaini kuwa soko hilo lina nyufa zilizotokana na ujenzi ulio chini ya kiwango kisha kuzibwa kwa saruji ili kuficha ubovu huo kabla ya kukabidhiwa.
 
Kutokana na soko hilo kutojengwa kwa ubora uliokuwa ukitakiwa, Mafundi wa soko hilo wameuambia mtandao huu wa www.jamiiyetu2012.blogspot.com kuwa lawama za soko hilo kutokuwa bora zinapaswa kuwaendea wahandisi wa Serikali wa Jiji la Mbeya ambao mara kwa mara wamekuwa wakifika eneo la ujenzi na kuishia ofisi za mkandarasi kisha kuondoka.
 
 
Walisema kuwa uozo huo upo tangu soko linaanza kujengwa lakini hakuna kiongozi wa Serikali ambaye amewahi kuwauliza hata mafundi kwa siri ili kujua uhalisia wa ujenzi wa soko hilo.
 
 
Kutokana na uzalendo wa mafundi hao, waliamua kumwandikia barua ya uhalisia wa soko hilo Katibu mkuu wa tawala za mikoa na Serikali za mitaa ‘’Tamisemi’’ wakieleza kuwa soko hilo halina ubora na endapo Serikali italipokea maafa yatakayotokea lawama ziwe juu ya Serikali.
 
 
Barua hizo ambazo nakala zake zipo, zimeeleza kuwa kama Serikali ni sikivu itafute wataalam wake na kukagua kwa kuchimbua Msingi wa Soko hilo ambapo soko hilo halina mhimili wa kuunganisha jengo zima (Ring Bim) ili kulifanya kuwa imara.
 
Mafundi hao wamesema wakati wa kufanya jambo hilo wawepo kwa ajili ya ushahidi pamoja na waandishi wa habari ili kusiwepo hali ya kulindana na mazingira ya Rushwa kwa watendaji hao wa Serikali na kama kiunganishi hicho kitakutwa, Serikali iwapeleke mahakamani.
 
 
Barua moja ambayo imeandikwa na fundi Saimon Uledi ambaye ni mmoja wa mafundi waanzilishi wa soko hilo, kwenda Tamisemi iliandikwa June 6, 2011 na kueleza undani wa kutokuwa na ubora wa ujenzi wa soko hilo na kuhofia kuwa endapo kutatokea tetemeko basi wananchi watakaotumia soko hilo watapata maafa makubwa.
 
‘’Nakuomba Katibu Mkuu fuatilia ujenzi wa soko la Mwanjelwa kuanzia tofali la kwanza chini ya Ardhi ili upate uhakika kama Ring Bim lipo, Maslahi ya wafanyakazi, mikataba mibovu isiyo na picha na ubora wa jengo kwa ujumla’’ imesema moja ya haya ya barua hiyo.
 
Kutokana na barua hiyo, Tamisemi iliamua kumwandikia Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya barua yenye kumbukumbu namba MCC/M.50/17/VOL II/226 ya Julai 7,2011 ili aweze kuzitolea ufafanuzi tuhuma hizo na nakala yake ikaenda kwa Katibu tawala wa mkoa wa Mbeya.
 
Mbali na barua hiyo, Tamisemi ilimwandikia barua katibu tawala wa mkoa wa Mbeya Septemba 23,2011 yenye kichwa cha barua Ujenzi wa  soko la Mwanjelwa Mbeya kutokuwa na ubora ikimweleza kuwa kuna malalamiko ya soko hilo kuwa na ujenzi hafifu ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mkanda wa chini (Ground beam) kwenye jengo hilo.
 
‘’ Kwa kuwa jengo hilo ni kwa matumizi ya umma na dhamana ya ujenzi wake unasimamiwa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, yaani Halmashauri ya  Jiji la Mbeya, OWM-TAMISEMI ilifanya mawasiliano na Mamlaka hiyo ili kupata taarifa za awali na vielelezo vya kiufundi ili kujiridhisha na uwepo wa ‘’ground beam’’kwenye michoro ya usanifu ‘’architectural’’ na mhimili ‘’structural.
 
‘’Halmashauri ya jiji la Mbeya iliwasilisha maelezo kuwa malalamiko hayo sio ya kweli na kwamba ujenzi umezingatia taratibu zote na viwango vya ubora vinazingatiwa’’ imesema barua hiyo yenye kumbukumbu namba HA.78/225/01/07/13
 
Aidha Tamisemi imemuomba Katibu tawala wa mkoa wa Mbeya kufuatilia kwa karibu ujenzi wa soko hilo na kufanya ukaguzi maalum ili kubainisha ukweli kuhusu tuhuma zilizotolewa na mafundi hao.
 
Kutokana na kile kilichoonekana kuwa Serikali inachelewa kuchukua maamuzi dhidi ya wahusika wa ujenzi wa soko hilo licha ya kuwepo ushahidi wa wazi, mafundi hao walimwandikia barua katibu mkuu wa ofisi ya Waziri Mkuu Desemba 1, 2011 wakieleza kuwa endapo wakikuta mhimili wa jengo hilo wapo tayari kufungwa, lakini hawajapatiwa majibu.
 
Mafundi hao baada ya kuona barua zao zinapuuzwa, waliamua kutoa taarifa katika ofisi za Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya kwa ajili ya usalama wao ambapo taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zimethibitisha kuwepo kwa taarifa hiyo na kwamba baadhi ya vigogo wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya tayari wamehojiwa.
 
Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi (Chadema) ambaye pia alipelekewa barua ya malalamiko ya ujenzi huo alipotafutwa kwa njia ya simu jana alikiri kupokea malalamiko hayo na kwamba analitafutia ufumbuzi wa kisayansi tatizo hilo na na mikataba kwa kuzijulisha ngazi zingine za Serikali.

No comments:

Post a Comment