Saturday, September 1, 2012

Sauti kutoka Nyikani Chadema na hadithi ya Brown ashika tama


  KATIBU WA CHADEMA TAIFA DR.WILBROAD SLAA.

LEO nazungumza na ‘’wenye’’ chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wala sitaki kuzungumza na wapambe maana najua tofauti ya dhamira ya Bwana harusi halisi na msindikizaji kwamba huwa tofauti.
 
Katika maandalizi ya sherehe za harusi anayetakiwa kuoa ama wazazi wake wakiwaita watu ili wawe wajumbe katika kamati mbalimbali za harusi hiyo huwa wanaulizwa kuwa wana kiasi gani cha fedha ili mipango iendelee na hapo huwa hawaulizi wapambe wa Bwana harusi au Bibi harusi kuwa wanacho kiasi gani na ndiyo maana nasema nazungumza na wenye chama na wala si waandamanaji.
 
Mfumo wa vyama vingi hapa nchini umeendelea kuota mizizi huku wengi wakiacha katiba zao nyuma na wao kuwa mbele kwa kusaka kwa kila aina madaraka badala ya kusaka na kudumisha demokrasia na elimu ya uraia kwa wananchi.
 
Wakati wanasaka vyeo hivyo huwa hawawi wazi sana kusema kinachowasukuma bali wanaendelea kuwajaza wapiga kura hasira ambazo wengi wao hujikuta wakipata hata madhara kwa kupigana na wenzao ambao wanahisi kuwa hawajajaa vema hasira hizo huku Vigogo waliowajaza hasira na kusingizia kuwa wanaosababisha maisha yao kuwa magumu ni CCM, lakini wao wanagonga bilauli za juisi pamoja na viongozi wa CCM hao hao.

Na hapa siseme wazi kwa msisitizo kuwa hakuna kitu kibaya kuishi kwa kutegemea fikra za wenzako maana kuna siku watakuja kukujaza ujinga kuwa umasikini uliona umesababishwa na jirani yako wakati ukweli ni kwamba wewe ni mvivu na mwenzako anachapa kazi.
 
Sauti yangu kutoka hapa Nyikani inataka kuwakumbusha jambo wenye Chadema kuwa naamini kabisa kuwa wengi wao wanakumbuka kilichokuwa kitabu cha Hadithi katika shule za Msingi ambapo katika kitabu hicho kulikuwa na hadithi isemayo ‘’Brown ashika tama’’
 
Kwa wale ambao hawakubahatika kukisoma kitabu hicho walipoanza masomo yao hasa vijana ambao wanajiita wanaharakati niwakumbushe hadithi hiyo kuwa ilikuwa ikihusu Kijiji cha Nsalala Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.
 
Hadithi hiyo ilikuwa ikimhusu Mzee Kasunga na Mzungu aliyekuwa akiitwa Brown ambapo mzungu huyo alifika Kijijini hapo na kuanza kuuliza ni jinsi gani ukoloni uliondoka nchini Tanzania.
 
Baada ya kuuliza swali hilo , Mzee Kasunga akamchukua Brown na kuanza kumsimulia jinsi Tanzania ilivyoweza kuondosha ukoloni hapa nchini hivyo mazungumzo yalipokuwa yamekolea yalimgusa sana yule Mzungu aliyeitwa Brown.
 
Mzungu huyo alipokuwa akiendelea kusikiliza kwa umakini, kuna mpiga picha aliwapiga picha wakiwa katikati ya mazungumzo huku Brown akiwa ameshika shavu lake hivyo hadithi ile kutokana na maudhui yake na picha ya Mzungu kushika shavu ikapewa jina la ‘’Brown ashika tama’’.
 
Hadithi hiyo inanikumbusha jambo ambalo nalishabiisha na mambo yanayotokea kwenye siasa za hapa nchini husani katika maandamano yanayofanywa na Chama cha demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo kila baada ya maandamano hayo mtu ukisimuliwa jinsi yanavyoratibiwa na matokeo yake inakubidi ushike shavu na ndiyo maana nasema kuwa Chadema na hadithi ya Brown ashika tama
 
Sihitaji kuzungumzia matukio mengi au maandamano mengi ya Chadema yaliyowahi kutokea pamoja na matokeo yake katika kila maandamano ya chama hicho chenye usajili wa kudumu nchini Tanzania , bali nataka nikumbushe kidogo tukio la Hivi karibuni la mkoani Morogoro.
 
Wakati wa maandamano hayo ya Chadema kuna kijana ambaye hakuwepo kwenye maandamano alikutwa amefariki na baadhi ya vyombo vya habari vikasema kuwa vimeambiwa kuwa aliuawa na Polisi na wala havikusema kuwa alisadikika kuuawa na Polisi! Inasikitisha sana na kwa mtu mwenye kutafakari lazima ashike tama kwanza.
 
Ilielezwa kuwa kijana huyo aliuawa sehemu ambayo hakukuwa na maandamano wala askari Polisi bali waliojiita mashuhuda walisema kuwa watu wanaosadikika kuhusika na kifo cha kijana huyo walivaa mavazi yanayofanana na yale ya Polisi na hapo kwa upande wangu na wengine maelezo hayo yakatupelekea kuhisi kuwa yawezekana walikuwa wahalifu waliovaa mavazi ya Chadema yanayofanana na Polisi hakika ni huzuni.
 
Lakini uhalifu wa namna hii unaonekana kuwa ni mitaji ya kisiasa kwa baadhi ya wanasiasa na hapa napata wasiwasi kuwa kuna siku viongozi hawa waliotamka kuwa Polisi walihusika katika kifo cha yule kijana pale Morogoro kuna siku wataandamana na kupita karibu na eneo la Hospitali kisha watatangaza kuwa wagonjwa waliokufa siku hiyo wameuawa.
 
Ndiyo, kwasababu kwa sasa Jeshi la Polisi limekuwa jalala la kutupia lawama zote za kisiasa ili washindwe kuaminika katika jamii, hakika nasema katika hili Chadema haikwepi kufananishwa matokeo ya siasa zake na hadithi ya Brown ashika tama.
 
Nasema Chadema haikwepi kufananishwa na hadithi ya Brown ashika tama kwasababu kinachopandwa ndicho kinachoota na hapa mkumbuke kuwa umefika wakati wa kurejesha mbegu bora katika Taifa, Mbegu ya upendo, amani, Heshima kwa watu wa rika zote na maeneo yote.
 
Lakini kama haitakuwa hivyo vijana hawa mliowapandikiza chuki mnapokuwa kwenye maandamano na kwasababu hawajui nia yenu thabiti ya kufanya maandamano hayo wanakurupuka na kufanya kila wanaloona ni jema kwa kile wanachodai kuwa Chadema kina wanasheria wengi hivyo watawatetea hata wakikamatwa.
 
Katika jambo hilo nawalilia Chadema na kuwauliza kuwa je mnaukumbuka wimbo ulioimbwa na kwaya ya Ambassador of Christ toleo la pili unaosema kwanini umeyaruhusu?
 
Kabla damu za watu hazijawalilia, Nimeshika tama huku Nyikani nawauliza nyie wenye Chadema kuwa kwanini mnayaruhusu?
 
Kwa kuyaruhusu mengi mnayoyaruhusu yakiwemo maandamano yenye vibali na hata ambayo yanakuwa hayana vibali kama yale yaliyozuiliwa mkoani Iringa Juma lililopita imefikia mahala hata baadhi ya watumishi wakiwemo walimu wakijipa moyo kwa kusema kuwa wao wapo kila mahala katika nchi hii hivyo CCM itakiona cha moto kwasababu eti wanafahamu njia nyingi za ushindi, je nayo haya mmeyaruhusu?
 
Kwa kumalizia, nizungumze kifalsafa kidogo cha elimu ya kiupe upe hasa ukizingatia kuwa nimekulia huku Nyikani, sauti yangu iwafikie na muelewe kuwa mwanadamu hawezi kubadilika kuwa maji na mkitaka kujua hili huko mjini mliko, kaeni jikoni hata kwa wiki moja lakini hamtakuwa Sufuria hata siku moja bali mtatoka mkiwa watu mliopauka kwa moshi.
 
Pili niwajulishe kuwa huku nilipo Nyikani, kuna nyoka aina nyingi na mfano mzuri niwaambie kuwa Binadamu anao uwezo wa kumfukuza Nyoka wa Kijani akiwa kwenye majani awezavyo, lakini Nyoka huyo wa Kijani akifika kwenye mchanga hawezi kukimbia bali hugeuka na kung’ata na akikung’ata hakuna dawa ya sumu yake, hivyo Chadema mimi siwaruhusu naogopa watu watashika tama.
 
Mbali na Nyoka huyo pia kuna Nyoka anaitwa Kifutu ambaye ni Nyoka mpole sana unaweza kumkalia ila unapokuwa juu yake usijigeuzegeuze maana akishtukia kuwa wewe ni adui na unamsumbua sumbua lazima akung’ate na akikung’ata, sehemu ile ambayo imeng’atwa kila mwaka ifikapo tarehe uliyong’atwa itakuuma ili ukumbuke. Poleni wasomaji wangu wa safu hii kwa kushika tama.
 
Kupitia makala haya nawakumbusha mnaojua vema mipango ya sirini ya Chadema mbali na mashabiki, umefika wakati kujiepusha na historia ya hadithi ya Brown ashika tama, fanyeni hivyo kwa ukumbusho kama mnavyojiepusha kutoandaa maandamano mjini Moshi maana pale kuna familia zenu hakika nami nitaungana nanyi na kuimba wimbo wa kutoyaruhusu kote nchini ili kwa pamoja utupite mbali wimbo utakaoimbwa kuwa ‘’Kwanini mmeyaruhusu’’.

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa simu 0754 440749, barua pepe kalulunga2006@yahoo.com
 

No comments:

Post a Comment