Wednesday, September 5, 2012

DK. SLAA NA WENZAKE WADANDIA KINGUVU MAZISHI YA MWANGOSI, MBEYA

 VIONGOZI wa CHADEMA wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dk.Willbroad Slaa, wametuhumiwa kulazimisha kinguvu, kushiriki mazishi ya aliyekuwa mwandishi wa kituo cha Channel Ten, mkoa wa Iringa marehemu Daud Mwangosi.

Marehemu Mwangosi aliyefariki katika vurugu, zilizobababishwa na CHADEMA eneo la Nyororo, alizikwa Jumanne ya wiki hii, katika kijiji cha Busoka, wilayani Rungwe huku kundi kubwa la wafuasi wa CHADEMA, likihudhuria mazishi hayo.

Inaelezwa licha ya kuambiwa msiba huo siyo wa kisiasa, hivyo hawatakiwi viongozi hao wala wanachama wa CHADEMA, lakini walilazimisha kushiriki kwa nguvu, na hata mwili wa marehemu ulipowasili Tukuyu mjini ukitokea mkoani Iringa, walilazimisha kuingia kinguvu kwenye gari hilo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Iringa, Francis Godwin, alisema kuwa tangu wakiwa mjini Iringa, aliwatangazia wazi CHADEMA kuwa msiba huo unawahusu waandishi wa habari na siyo wanasiasa.

“Tulianza kukwaruzana tangu hatujaondoka mjini Iringa, kwani wakati tunatangaza taratibu za kusafiri, nilitumiwa ujumbe na viongozi wa CHADEMA, kuwa nitangaze msafara huo utaongozwa na Dk.Slaa, lakini niliwakatalia kuwa huo siyo msiba wa mwanasiasa bali ni mwanahabari hivyo hilo halitawezekana” alisema Godwin.

Godwin alisema aliwaeleza wazi viongozi wa CHADEMA, kuwa kama wanataka kwenda kushiriki mazishi hayo basi ni vyema watafute taratibu nyingine za kufika wilayani Rungwe, lakini siyo kung’ang’ania waongozane na mwili wa marehemu, kitu kilichowakera viongozi hao.

Aliongeza kuwa walishangazwa walipofika Tukuyu mjini, kundi la vijana wafuasi wa CHADEMA walilifuata gari walilokuwemo waandishi wa habari kutoka mkoa wa Iringa ambamo ndipo mwili wa marehemu Mwangosi ulikuwemo na kuamua kuingia kinguvu.

Kwa mujibu wa Godwin, walipojaribu kuwakataza vijana hao wa CHADEMA, iwapo kuna mtu atawakatalia kuingia basi watambue wazi kuwa damu itamwagika hali iliyowafanya washindwe kuwazuia kwa kuogopa kuanzisha vurugu zisizo na msingi.

Aidha, katika kuonyesha kukerwa na hali hiyo iliyojitokeza, akizungumza wakati wa mazishi hayo yaliyofanyika kijiji cha Busoka, wilayani Rungwe, Godwin alisema hakuwahi kusikia marehemu Mwangosi akisema kuwa yeye ni mwanachama ama mfuasi wa chama chochote cha siasa.

Godwin alisema:”Ninachokifahamu mimi ni kuwa marehemu Mwangosi, alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Iringa, hivyo hatutegemei msiba huu kuanza kuingizwa itikadi za kisiasa”.

Aliongeza kwa kulitaka Jeshi la polisi kuwa hata kama marehemu Mwangosi, alifanya kosa lililopelekea akutwe na mauti hayo alipaswa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na siyo kufa aina ya kifo hicho cha kufa kwa bomu la machozi.

Katika kuonyesha kuwa kauli hizo ziliwachoma CHADEMA, Dk.Slaa aliposimama kuzungumza na wananchi, alisema anachofahamu yeye ni kuwa msiba hauna rangi, kabila wala dini.

Dk.Slaa aliongeza hivyo anapenda kutumia nafasi hiyo kukemea kauli za ubaguzi zilizotolewa, kwani CHADEMA wameenda kushiriki msiba huo kutokana na mahusiano waliyokuwa nayo na marehemu.

“Wakati tunaondoka mkoani Iringa kuja huku Rungwe-Mbeya, kuna kitu kilitokea ambacho kilitukwaza na sitapendi kukizungumza hapa…nimemjua marehemu Mwangosi alikuwa mtu wa haki na alikuwa akipinga vitendo vya kifisadi” alisema Dk.Slaa.

Aidha, taarifa zaidi zinaeleza kuwa wakati wa mazishi, Dk.Slaa alimfuata Godwin na kumueleza kuwa amemsamehe kwa yote aliyoyafanya hali ambayo ilimlazimu naye (Godwin), kumjibu kuwa hajafanya kosa lolote linalostahili asamehewe.

No comments:

Post a Comment