Wednesday, September 5, 2012

CHADEMA:Tunaomba Rais Jakaya Kikwete Awawajibishe Polisi

Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Chadema na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika akionesha picha ya polisi wakizingira Ofisi ya Tawi la chama hicho katika Kijiji cha Nyololo, Mufindi iliyochapishwa na gazeti la Tanzania Daima Jana
---

DAR ES SALAAM, Tanzania
 
CHAMA cha Demokrasi na Maendelea (Chadema), kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwasimamisha kazi vigogo wote wa Jeshi la Polisi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa mbalimbali za uongo kuhusu mauaji ya mwandishi Daudi Mwangosi, ama awatake wajiuzuru nyadhifa zao, kupisha uchunguzi.
 
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, aliwataja vigogo hao wa polisi kuwa ni Kamanda wa Operesheni wa Polisi, Paul Chagonja na RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda
 
Wawili hao kwa mujibu wa Mnyika, kwa nyakati tofauti walidai kuwa marehemu alifikwa na mauti baada ya kuchoropoka kutoka kwa kundi la wafuasi wa Chadema na kukimbilia mikononi mwa Polisi na ghafla kulitokea mlipuko wa bomu la machozi uliosababisha kifo chake, jambo ambalo sio la kweli.
 
Mnyika alisema maneno hayo yanayotofautiana na kuyaita kuwa ni  ya uongo ukizingatia kwamba picha mbalimbali zimeonesha ikiwemo waandishi waliokuwemo eneo la tukio kutoa ushuhuda wao.
 
 
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi huyo alisema ipo haja ya vigogo hao kung’oka kupisha uchunguzi, ili uweze kufanyika kwa haki na kuongeza kwamba Rais atumie madaraka yake kuhakikisha askari saba wanaoonekana katika picha 'wakimshughulikia' marehemu kukamatwa haraka na kuhojiwa ni nani alifyatua bunduki, kwa namna gani na vigogo gani walitoa amri hiyo.
 
Kwa mujibu wa Mnyika, Polisi imekuwa na tabia ya kukamata raia wanaokuwa eneo la tukio pindi kunapotokea mauaji kama hayo, hivyo ni wakati sasa wa Polisi wanaoonekana katika picha wakimshambulia marehemu Mwangosi nao kukamatwa.
 
Aidha alilitaka Jeshi la Polisi nchini lisitumie vibaya fedha za walipa kodi kwa kuchunguza nani alihusika na mauaji hayo wakati wauaji wanaonekana wazi kwenye picha za aina tofauti, badala yake  kinachotakiwa na wao kuhojiwa nani aliwaamuru kufanya mauaji hayo ya kinyama.

No comments:

Post a Comment