Monday, September 10, 2012

Poleni waandishi na Polisi, Hongereni wanasiasa, nakugomea Dr, Slaa

NASHINDWA kuyazuia machozi yangu yanapobubujika na kudondoa kwenye kope za macho yangu hasa ninapokumbuka kifo cha Mwandishi Daud Mwangosi na watanzania wengine waliokufa na kujeruhiwa kwenye mikutano ya kisiasa hapa nchini kwetu Tanzania.

Nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wote wakiwemo wanataaluma wote wakiwemo waandishi wa habari na askari Polisi Tanzania walioumia na wanaotarajiwa kuumizwa katika mikutano ya wanasiasa wetu kupitia ‘’Chama cha Migomo na matatizo yasiyokwisha’’ huku Polisi wakikosa mtu wa kuwasemea na kuendelea kuumizwa na kutukanwa majukwaani.

Sitaki kuorodhesha orodha ndefu ya matukiom ya kisiasa yaliyowahi kutusikitisha wengi hasa wananchi na askari polisi wanapoumizwa na hata vifo kutokea kutokana na ukaidi wa wanasiasa wenye uchu wa madaraka hapa nchini.

Nawapa ‘’Hongera’’ sana wanasiasa mnaaona ni fahari mioyoni mwenu kuona damu za watanzania zinamwagika na wengine wakipa ulemavu katika mikutano yenu ili tu ninyi mpate nafasi ya upangaji  pale Ikulu. Hongereni sana lakini mjue kuwa damu hizo zitakuwa juu yenu na watoto wenu.



Kama nilivyoshindwa kujizuia kutokwa na machozi vivyo hivyo nakosa kujizuia kuwaza vifo na majeraha vinavyotokea kwenye mikutano ya wanasiasa kuwa si kafara.

Naomba usilie msomaji wangu, futa machozi hata kama wewe unajua jambo hili kwa undani zaidi kikubwa utambue kuwa maisha ni safari ndefu isiyokuwa na likizo.

Kutoka hapa Nyikani naleta matumaini mapya kwenu  na kwa pamoja tukumbuke kuimba wimbo wetu wa kuwasha mwenge huku tukikumbuka maneno aliyoyatamka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Baadhi ya maneno ambayo aliyatamka Mwalimu Nyerere alisema kuwa Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka Mlima Kilimanjaro umulike hata nje ya mipaka yetu na ulete Tumaini.

Pale ambapo hapana matumaini, Upendo mahala ambapo pana chuki, Heshima ambapo pamejaa dharau.

Uhalisia wa maneno hayo ya Mwalimu wakati wa kuwasha Mwenge wa uhuru mwaka 1962 sasa unaonekana ambapo kwa sasa bila kutafuna maneno ni kwamba dharau zimezidi kwa watawala wetu na watu wanaoongoza dharau hizo ni wale ambao kila kukicha wanapaza sauti kuwa Mwenge ufutwe.

Wanapiga kelele na kupaza sauti zao ili kuendeleza dharau zao katika jamii na wanajua kuwa Mwenge unawakosesha amani mioyoni mwao na kushindwa kuendeleza dharau kwa watawala waliopo madarakani huku Mwenge ukipita kila kona na kufungua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanywa na wananchi wakati wao wanasema kuwa katika nchi hii hakuna kinachofanyika ‘’wao wanawaza maandamano tu’’

Mwenge ambao unaleta matumaini kwa wale waliokata tamaa na kujua propaganda za kuwafinyanga fikra zao ili waamini kuwa Serikali haifanyi lolote, umekuwa sumu kwao maana hata Viongozi au wakimbiza Mwenge wameendelea kukemea utengano wa kikabila, Rangi na uasi wa aina yeyote katika nchi yetu na huo umekuwa mwiba kwao.

Mfano mzuri wa wtu hao ambao mimi binafsi na baadhi ya waandishi wa habari nchini Tanzania tumetangaza rasmi kugoma kuandika habari zinazomuhusu Dr. Wilbroad Slaa kutokana na kutoridhishwa na mambo yake.

Kwa muda mrefu Dr. Slaa amekuwa chanzo cha mambo mengi hasa ya kutotii sheria bila shuruti na kwa kuonesha kile anachokiamini kuwa yeye ndiye yeye katika nchi hii ameamua na kujiridhisha kuwa anaweza kuwashika masikio hata waandishi wa habari kwa kufanya lolote hata kuingilia taaluma yao.

Nakumbuka Tarehe 4.09.2012 pale katika Kijiji cha Busoka kata ya Itete wilaya ya Rungwe (Tukuyu) mkoani Mbeya wakati wa Mazishi ya Mwandishi Daud Mwangosi ambapo Dr. Slaa aliamua kujivika umwamba na kujifanya yeye ni zaidi ya waandishi wa habari.

Katika mazishi ya Mwangosi Kaimu Katibu wa chama cha waandishi wa habari mkoani Iringa Mpiganaji Francis Godwin alisema kuwa tangu mwili wa Mwangosi ukiwa Iringa alipobaini kuwa Chadema ‘’walifurahia’’ kuuawa Mwangosi, walitaka kiuubeba mwili wa marehemu na kuhodhi msiba huo, aliaqmua kutangaza kuwa Msiba huo si wamwanasiasa bali ni wa-Mwandishi wa habari jambo ambalo liliwaudhi sana Chadema.

Mpiganaji mwenzangu Francis Godwin ambaye watu wengi wananichanganya naye mimi Gordon Kalulunga, alipofika na mwili wa marehemu Tukuyu aliwatangazia tena wananchi kuwa msiba huo haukuwa wa wanasiasa.

Baada ya kuona Francis anaendelea kukomelea msumari huo wa moto kwa wanasiasa akiwemo Dr. Slaa, Chadema hawakuridhika maana walijua kuwa kifo na maiti ya mwangosi ni moja ya vitega uchumu vya siasa zao kama walivyozoea.

Dr. Slaa alipoinuka akasema kuwa mwandishi huyo ingawa hakumtaja jina, alidai kuwa hajui alitendalo na amemsamehe kwasababu yeye binafsi alikuwa na mahusiano mema na Mwangosi tangu akiwa Mbunge na mambo mengine ambayo hakuweza kuyataja.

Ni utovu wa nidhamu kwa mwanasiasa kama Dr. Slaa anayehisi kuwa anaheshimiwa halafu yeye akiwa hataki kujiheshimu.

Prof. Mark Mwandosya alikomelea msumariu katika mazishi hayo na kutamka wazi kuwa ni upuuzi kujitafutia umaarufu katika matatizo ya watu hasa msiba.

Labda mimi na wenzangu nitamke rasmi kuwa natoa tamko la kutokuwa na imani na Dr. Slaa na ninasusia kuandika habari zake kutokana na dharau zake kwa waandishi wa habari huku akiamini kuwa yeye ni mungu mtu anayeweza kunye4nyekewa na kila mtu. Ni upuuzi mkubwa.

Sitoi msimamo huo kwasababu Mwangosi ni kabila langu la watu ambao ni wenye msimamo duniani bali natoa tamko hili kwa kuwa Chadema naamini kuwa ni chanzo cha kifo cha Mwangosi na kutotii sheria bila shuruti kwa wanasiasa wa Chadema hivyo fikra zangu ambazo naamini ni sahihi zinatamka kwa herufi kubwa kuwa kwasababu wameona kifo cha Mwangosi ni mtaji wa kisiasa kwao sina imani nao.

Katika makala haya kama ilivyo kawaida ya wahuni wachache natarajia kupata matusi kupitia sms na vitisho huku wakisaqhau kuwa siku za kuishi kwangu anazijua zaidi Mungu aliyerumruhusu Mama yangu mzazi kuzaliwa kwangu.

Msipate shida kufikiri zaidi juu ya uhai wangu maana naamini ukweli huu utadumu zaidi kuliko uhai nilio nao, na ninamalizia kwa kusema kuwa waandishi wa habariu hata kama tumeahidiwa kuwa tutakuwa wapiga picha wa Rais wa kufikirika ajaye, tutambue kuwa atakayekuchoma kwa kalamu akiingia madarakani atakuchoma kwa risasi kama hivi atumiavyo Dr. Slaa kutu,ia vyombo vya habari kuikuza Chadema, namaliza kwa kusema Poleni waandishi na Polisi, Hongereni wanasiasa, nakugomea Dr, Slaa.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0754 440749

No comments:

Post a Comment