Friday, August 31, 2012

DC MBARALI MBEYA ANUSURIKA KUUMIZWA NA WANAFUNZI WA CHUO CHA UUGUZI CHIMALA

Na Venance Matinya, Mbeya.
MKUU wa Wilaya ya Mbarali Gulamu Hussen Kiffu  amenusurika kuumizwa na wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha Chimala kilichopo Wilayani humo baada ya kuvamia gari lake na kuvunja vioo,kutoa upepo wa matairi  kutokana na Serikali kufunga chuo hicho kwa kutokuwa na hadhi ya kudaili wanafunzi.

Kutokana na vurugu hizo zilizotokea chuoni hapo juzi jioni, Jeshi  la polisi Mkoani Mbeya linawashikilia wanafunzi  sita    akiwemo Mkuu wa Chuo  hicho  Francis Mtega  kwa  tuhuma za kuhamasisha vurugu  zilizopelekea  kuharibu gari la Mkuu wa Wilaya ya  Mbarali. 

Kamanda wa polisi Mkoani hapa Diwani Athuman  alisema  baada ya mkuu wa wilaya kuongozana na baadhi ya viongozi wa serikali  hususani kamati ya ulinzi na usalama wilaya kwa lengo la kutaka kujua sababu za chuo hicho kuendelea kufundisha wakati serikali ilitoa agizo kifungwe ndipo hapo walipovamiwa na wanachuo hao.

Alisema   tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya kuwasili Chuoni hapo kwa  lengo la  kuzungumza na uongozi wa chuo ndipo baadhi ya wanafunzi  walivamia gari la Mkuu wa Wilaya na kuanza kuvunja vioo kwa kutumia mawena kisha kutoa upepo kwa malengo yasiyojulikana.

Kamanda Athumani alisema tukio hilo linaonesha ni mpango uliokuwa umepangwa na uongozi wa Chuo  kwa muda mrefu kwani serikali ina malengo mazuri kwa watanzania  na lengo kuu ilitaka chuo hicho kisajiliwe  ili kitambulike  na Serikali na kuweza kutoa wauguzi walio na sifa na kuwawezesha kupata ajira itakayotambulika serikalini. 

Aliongeza kuwa  kitu cha kushangaza ni madaraka aliyonayo mkuu wa chuo hicho ambapo yeye mwenyewe ni mwalimu na mhasibu na kwamba kulikuwa hakuna sababu ya kufanya vurugu bali  kilikuwa ni kitu cha kutoa vielelezo vya udaili wa chuo.

Alisema katika uchunguzi wa awali  umebaini kuwa chuo hicho kimeanza muda mrefu na tayari  kimeweza kutoa wauguzi katika Nyanja mbalimbali  bila ya serikali kutambua  kama hakijasajiliwa na hakitambuliki.
  
“ Kutokana na vurugu hizo  wanafunzi  32 wanashikiliwa na Jeshi la P[olisi ambapo kati ya hao watano ndio waliobainika kuhusika na vurugu hizo na wanatarajiwa kufikiswa  mahakamani wakati wowote kujibu tuhuma zinazowakabili ili sheria ichukue mkondo wake ili iwe fundisho kwa wengine” alisema Kamanda huyo.

Aliwataja  wanaoshikiliwa na polisi kuwa ni Mkuu wa Chuo  Francis Mtega, Steven Mapunda (19), Isaya Katuwa (23) , Lugano Mwalupasya (22), Emmanuel Bukuku (24)  ambao wanatarajia kufanya mtihani wiki ijayo ya kuhitimu mafunzo ya uuguzi. 

Kwa upande wake  Mkuu wa Wilaya ya Mbarali  Gulamu Hussen Kiffu alikiri kutokea kwa vurugu hizo  zilizotokana na uamuzi wa serikali kufunga chuo hicho  kutokana na kutokuwa na sifa ya kufundisha na kudaili wanafunzi  wa fani ya uuguzi kwani kilikuwa hakina hati ya utambulisho wa usajiri serikalini.

Kiffu alisema kuwa baada ya serikali kutambua tatizo hilo ndipo walipo mwita  Mkuu wa Chuo  hicho Francis Mtega katika kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ambapo aligoma kuhudhuria na kueleza kuwa yeye anaendelea kufundisha ndipo walipolazimika kufika chuoni hapo.

No comments:

Post a Comment