Friday, August 31, 2012

JIJI LA MBEYA LALALAMIKIWA ''UFISADI'' ARDHI

* Afisa anayelalamikiwa ahamishwa badala ya kuwajibishwa
 
SIKU chache baada ya wananchi wa Jiji la Mbeya kuwalalamikia baadhi ya maafisa Ardhi wa Jiji hilo kujikadilia mapato kidogo ya nyumba zao huku wakiwapandishia gharama wananchi wa kawaida, tuhuma zingine nzito za uporaji wa ardhi zimeibuka dhidi yao huku wakidaiwa kuendelea kulindwa.
 
Hali hiyo imebainika baada ya wananchi hao kumwandikia barua Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya makazi huku wengine wakimwandikia Meya wa Jiji hilo Athanas Kapunga kuwalalamikia maafisa wa Jiji la Mbeya kuwapora ardhi kwa mgogo wa Serikali kuchukua ardhi hiyo kwa matumizi maalum.
 
Barua ambazo zimenaswa na kuthibitishwa ni pamoja na barua ya wananchi wakazi wa mtaa wa Manga Veta kata ya Ilemi Mbeya Mjini ambao wamepeleka kero Wizarani na ofisi ya Rais –Ikulu kwa kile walichodai kuwa ni vitendo wanavyofanyiwa na ofisi ya Ardhi Jiji la Mbeya.
 
Barua hiyo ya Agosti 9,2011 imesema kuna mchezo mchafu umekithiri kwa watendaji wa Jiji la Mbeya kitengo cha ardhi ambao hujimilikisha maeneo kwa kutumia majina hewa kumbe viwanja hivyo ni vyao wenyewe na wakiulizwa wanasema kuwa ni sheria za mipango miji.
 
‘’Tuliletewa barua tarehe 13.06/2011 yenye kumb.Na. MCC/LD/M.13/VOLI. Iliyoandikwa na mwanasheria wa Jiji S.W.Mwangomale akishirikiana na mthamini wa Jiji Bi. Edina Mwaigomole akituamuru kuondoka eneo hilo ndani ya siku 14 wakidai kuwa Serikali imetenga eneo hilo kwa ajili ya soko wakati si kweli’’ imesema moja ya haya ya barua hiyo.
 
Barua hiyo imeendelea kusema kuwa katika barua hiyo ilionekana kuwa wananchi walikuwa tayari wamelipwa wakati hakuna mkutano wowote uliowahi kufanyika kwa ajili ya makubaliano ya kuondoka eneo hilo ambapo wananchi wameomba kuthibitishwa na kuoneshwa mtiririko wa malipo kutoka ofisi ya Jiji hali ambayo mpaka sasa imeshindikana kuthibitishwa.
 
Baada ya malalamiko ya wananchi, Wizara ya Ardhi, nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia barua ya Juni 25, 2012 yenye kumb.Na. EA 71/176/01H  iliyosainiwa na Kaimu katibu wa Wizara hiyo Verdiana A. Mashingia ilisema kuwa inashughulikia malalamiko hayo.
 
Wakati wananchi wa eneo hilo wakilalamikia idara hiyo ya Ardhi, wakazi wengine wa eneo la Gombe kusini kata ya Itezi jijini humo wameamua kumwandikia barua ya malalamiko Mstahiki Meya wa Jiji hilo wakiwalalamikia maafisa wa idara hiyo ya ardhi kuwa maeneo yao yameuzwa kwa watu wengine ili hali kuna nyumba zao za kuishi.
 
Barua hiyo ambayo imeandikwa Agosti 16, 2012 iliambatanishwa na nyaraka mbalimabli za mawasiliano na idara ya mipango miji na historia ya eneo hilo huku wakilalamikia pia matumizi mabaya ya madaraka na sheria kwa kujinufaisha nazo zinazowawezesha kuhalalisha ubovu na ubinafsi katika utendaji.
 
‘’Kupima maeneo ambayo tayari yamejengwa na kuwapa hati watu wengine na hivyo kuwaondoa wakazi asili kiuonevu kwa kuwa hawana uwezo kifedha na zoezi kunuka rushwa waziwazi. Kwa mfano kamati zikibatilisha na kubadili matumizi ya ardhi, maofisa wanakaa kwa nia ya kujinufaisha na kupanga watekeleze vipi na kwa kiwango gani’’zimesema haya za barua hiyo yenye kurasa tatu.
 
Eneo hilo ambalo lipo karibu na shule za St. Agrrey awali lilipangwa kuwa eneo la viwanda lakini likabadilishwa kuwa makazi ya watu lakini inaonekana kuwa baadhi ya maafisa ardhi (majina yanahifadhiwa) wanahusika kulihujumu.

Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Juma Idd alisema kuwa kuhusu suala la eneo la Manga analifahamu na analitafutia ufumbuzi kwasababu malalamiko ya wananchi ameyapokea na suala la Gombe kusini ameahidi kulitolea majawabu hapo baadae huku akisema kuwa Afisa Ardhi anayelalamikiwa amehamishwa.

No comments:

Post a Comment